Jumanne, 29 Novemba 2016

Taasisi ya kifedha ya Bayport imetoa msaada wa kompyuta 205

Na May Simba-MAELEZO.

Taasisi ya kifedha ya Bayport imetoa msaada wa kompyuta 205 zenye thamani ya Sh. Milioni 500 kwa ajili ya kuimarisha matumizi ya Teknolijia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli za Serikali.

Akizungumza mara baada ya kupokea msaada huo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki amesema kuwa kompyuta hizo zitasaidia kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali za Serikali.

Amesema kuwa kati ya komputya hizo, komputya 125 zitabaki kwenye Makao Makuu ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na zilizobaki 80 zitagawanywa kulingana na mahitaji ya Ofisi zake nyingine.

Waziri Kairuki ameongeza kuwa kompyuta hizo pia zinatarajiwa kutumika katika shughuli za usimamizi wa taarifa za watumishi na mishahara.

“Natoa wito kwa Taasisi binafsi nchini kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za kijamii ili kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi” Alisema Waziri Kairuki.

Aidha Waziri Kairuki ameiomba Taasisi ya kifedha Bayport kupunguza riba katika mikopo wanayoitoa, kuongeza kiwango cha fedha wanazokopesha watumishi wa umma ili kujiletea maendeleo yao wenyewe na Taifa kwa ujumla.

Ameongeza kuwa ni vema ikaongeza wigo wa utoaji wa mikopo ikiwemo mikopo ya viwanja, elimu na biashara.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bayport John Mbaga alisema msaada wa Kompyuta hizo zinatokana na kiu yao kubwa ya kushirikiana na Serikali katika kuboresha utendaji kazi wa watumishi wa umma kwa ajili ya kufanikisha huduma bora kwa Watanzania.

“Sisi jukumu letu ni kushirikiana na Serikali sambamba na kujitolea kwenye jamii kwa kusaidia mambo mbalimbali kwa ajili ya kukwamua wateja wetu kwa ujumla kwa kupitia sekta ya mikopo”.Alisema Mbaga.

Makabidhiano ya Kompyuta hizi ni sehemu ya kusheherekea miaka 10 ya huduma za Bayport ilipoanzishwa mwaka 2006.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni