Jumanne, 29 Novemba 2016

Profesa Muhongo, Waziri Wa Nishati Zambia Wakutana Kuzungumzia Bomba La Tazama

SeeBait
 Timothy Marko.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati wa Zambia, David Mabumba, wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu kuboresha Bomba la Mafuta la TAZAMA ili liweze kuwanufaisha wananchi wa Tanzania na Zambia kama ilivyokusudiwa.

Mazungumzo yao yaliyofanyika mapema leo, ofisini kwa Waziri Muhongo jijini Dar es Salaam, ni kufuatia makubaliano ya marais wa nchi husika, Dk John Magufuli na Edgar Lungu; kuhusu kuboresha zaidi Bomba la TAZAMA na Reli ya TAZARA.

Marais Magufuli na Lungu, walifikia makubaliano hayo jana katika mazungumzo rasmi yaliyofanyika Ikulu ya Dar es Salaam ambayo ni mojawapo ya shughuli mbalimbali zilizopangwa katika ratiba ya ziara ya siku Tatu (3) ya Rais Lungu iliyoanza nchini Jumapili, Novemba 21 mwaka huu.

Waziri Mabumba ambaye alifuatana na Ujumbe wa Viongozi na Maafisa waandamizi kutoka TAZAMA na wizarani kwake; aliafiki mapendekezo yaliyotolewa na Waziri Muhongo kuhusu namna pande hizo mbili zitakavyoshirikiana katika utekelezaji wa agizo la Marais wao ambayo ni pamoja na wataalam wa pande zote kukutana na kufanya majadiliano pamoja na kufanya ziara kukagua utendaji kazi wa Bomba hilo.

Aidha, Mawaziri hao walijadiliana kuhusu namna ambavyo Zambia itanufaika na gesi asilia iliyogunduliwa Kusini mwa Tanzania.

Kikao hicho pia, kilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini – Tanzania, akiwamo Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni