Alhamisi, 31 Oktoba 2013

UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU

1.    UTANGULIZI
Wizara imekusanya maoni ya Wadau wa Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika Mitihani ya Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA) kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi. Maoni ya wadau yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya alama vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani ya kuhitimu Kidato cha Nne na Kidato cha Sita umekuwa haufanani pamoja na kwamba mitihani hiyo yote ni ya elimu ya sekondari. Pia mfumo masuala mbalimbali ya mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa kuna miundo mikuu miwili katika mfumo huo.
Muundo wa Kwanza ni upangaji wa viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade Ranges) zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 – 60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na umezoeleka kwa walimu na wanafunzi wa elimu ya sekondari kwa ujumla.
Muundo wa Pili ni wa viwango vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya mwaka 2012 muundo wa viwango nyumbufu (flexible grade ranges) ulitumika. Katika muundo huu uwigo wa alama ulibadilika badilika kulingana na hali ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini kuanzia mwaka 2012, Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando (Fixed Grade Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa alama mgando ambapo: A = 80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0 – 34. Kwa upande wa Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B = 75 - 79; C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39. Mifumo hii ya Baraza haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa sehemu ya malalamiko katika sekta ya elimu na mafunzo.
Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA zitachangia asilimia hamsini (50%) na Mtihani wa mwisho utachangia asilimia hamsini (50%). Kwa upande wa Zanzibar, CA zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia arobaini (40%) na mtihani wa mwisho asilimia sitini (60%). Pamoja na kwamba Baraza halijawahi kuutumia mifumo hii tangu ilipowekwa, kumekuwa na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA kuchangia matokeo ya mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa watahiniwa wa kujitegemea (private candidates). Kwa sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa yakitumia alama za mtihani wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama utaratibu ambao unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza kielimu lakini anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa mtahiniwa.
Kwa mantiki hii, Wizara imedhamiria kufanya harmonization ya masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita ili kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau wote wa elimu ya sekondari. Lakini pia serikali imedhamiria kuhakikisha tathmini za wanafunzi katika ngazi mbalimbali zinakwenda sambamba na matarajio ya mitaala inayotumika na ambayo inahuishwa mara kwa mara ili iendane na wakati na mahitaji ya elimu katika ngazi mbalimbali.
2.    DHANA YA MITIHANI NA ALAMA
Mitihani hutumika kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo kupima endapo malengo ya kujifunza na kufundisha yamefikiwa na pia kubaini changamoto mbalimbali katika utoaji wa elimu katika ngazi husika. Kimsingi, mfumo wa mitihani ni jambo linalopangwa kwa kuangalia mambo mbalimbali ikiwemo hali halisi ya elimu katika ngazi husika. Mfumo unaweza kubadilika kulingana na elimu inavyoendelea kukua na mahitaji mbalimbali yanavyoendelea kujitokeza. Mtihani wowote lazima uwe na matokeo. Ili matokeo haya yapatikane, kila nchi imejiwekea utaratibu wa kuyapata matokeo hayo kulingana na malengo (objectives) ya mtihani husika.
Kitaalamu, mtihani una uhusiano mkubwa sana na mitaala (curricula) na mihtasari yake na jinsi mitaala hiyo inavyofundishwa na wanafunzi kujifunza (curricula instruction or delivery). Mitihani pia huwa inafanyika katika muda maalum na kwa hivyo kuna:
a)     mitihani kwa ajili ya kupanga wanafunzi katika makundi (streams) kulingana na umahiri wao (placement assessment),
b)     mitihani ya kubaini kama ufundishaji unakwenda vizuri na changamoto zilizopo ili kuchukua hatua rekebu kadri mwanafunzi anavyoendelea kukua kielimu (diagnostic assessment),
c)     mitihani ya kubaini ukuaji wa mwanafunzi kielimu (formative assessment) na
d)     mitihani ya kumaliza elimu katika ngazi husika (summative assessment).
Mara nyingi mitihani ya kundi (a) mpaka (c) inaunda kundi la CA wakati ile ya kundi (d) inaunda kundi la mtihani wa mwisho (final examination ama FE).
Ili upimaji ufanyike, ni lazima mtihani uwe na muundo stahiki wa alama (grading structure). Muundo huu hupangwa kulingana na maamuzi ya uwigo gani utumike. Kwa mfano, ngazi nyingi za elimu hutumia uwigo wa alama 0 hadi 100 na kuna sehemu nyingine uwigo wake ni 0 hadi 50. Kwa miaka mingi, uwigo wa alama kwa Kidato cha Kwanza hadi cha Sita hapa nchini umekuwa wa alama 0 hadi 100.
Pia, kimsingi, kuna mifumo miwili ya upangaji wa viwango vya ufaulu duniani katika kutunuku ufaulu. Baadhi ya nchi au mifumo hutumia viwango vinavyobadilika (flexible grade ranges) ambavyo hupangwa kwa kutegemeana na ufaulu wa watahiniwa katika somo husika. Nchi au mifumo mingine hutumia viwango visivyobadilika (fixed grade ranges) ambavyo hupangwa na nchi au mifumo husika vitumike kama kipimo cha ufaulu kwa masomo mbalimbali. 
Katika mitihani ya elimu ya sekondari, Tanzania ilifuata mfumo wa kutumia viwango vinavyobadilika (Flexible Grades) kuanzia mwaka 1973 hadi 2011. Hata hivyo, kwa madhumuni ya kuwawezesha wadau kujua viwango vya ufaulu vinavyotumika katika kutunuku matokeo ya mitihani ya taifa ya sekondari, Serikali iliamua kuanza kutumika kwa utaratibu wa viwango vya ufaulu visivyobadilika (Fixed Grades) kuanzia mwaka 2012. Suala kubwa lililokuwa limebaki lilikuwa ushirikishwaji wa wadau ili kuliweka wazi suala hili na kila mdau aweze kujua mfumo na miundo yake ikiwemo mfiko wa alama na maana yake katika kila kundi la alama.
3.    MAONI YA WADAU
Kabla ya kuwashirikisha wadau, Wizara iliunda Kamati ndogo kupitia taarifa mbalimbali na kutoa mapendekezo ya jinsi muundo wa alama katika mitihani ya Kidato cha Nne na Kidato cha Sita unavyoweza kuwa. Kamati hii ilifanya kazi hiyo na kutoa mapendekezo yake ambayo nayo yalipelekwa kwa wadau kwa ajili ya majadiliano zaidi. Wadau mbalimbali walishirikishwa katika kutoa maoni juu ya utaratibu mpya wa upangaji wa viwango vya alama na ufaulu.  Wadau hao ni pamoja na jukwaa la taasisi za elimu ya juu, chama cha wakuu wa shule za Sekondari nchini (TAHOSSA) wakuu wa vyuo vya ualimu vya umma, wamiliki na wakuu wa shule na vyuo visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), wakaguzi wa shule kanda, muungano wa wanafunzi wa Taasisi za elimu ya juu nchini (TAHLISO), viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, walimu, wanafunzi, wazazi, maafisa elimu Mkoa, Wilaya pamoja na maafisa taaluma wao, wadau kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,  Wanataaluma na Wanasiasa.
Maoni hayo yalikusanywa kupitia mikutano mbalimbali na kwa njia ya madodoso. Wadau wote walikubaliana kwamba mfumo nyumbufu wa alama siyo mzuri na hivyo taifa lihamie kwenye mfumo wa alama mgando katika mitihani mbalimbali.
Kwa jumla wadau walipendelea utaratibu wa upangaji makundi ya alama kwa kuzingatia muachano wa alama kumi kumi kutoka kundi moja hadi jingine. Hali hii inasaidia kuondokana na muundo ambao unawalundika wanafunzi wengi na mara nyingi wasiofanana katika uwezo wao kielimu katika kundi moja. Aidha wadau walipendekeza kiwango cha chini cha ufaulu mzuri kuwa Cna hii iwe sawa na alama 40.
Kwa upande wa alama endelevu, wadau pia walipendelea kuwa CA ichangie asilimia 40 katika matokeo ya mitihani ya kuhitimu ngazi husika ya masomo. Hata hivyo, wadau walitoa angalizo kwamba ni vyema kukawa na muundo na utaratibu mzuri wa kuzipata alama endelevu za mwanafunzi. Muundo na utaratibu huo unaweza kutumia mitihani ya Kidato cha Pili na ile ya mock ya Kidato cha Nne ambayo huwa inaandaliwa, kusimamiwa na kusahihishwa kwa umakini na weledi wa kutosha. Pia mwalimu naye asinyimwe fursa ya kuchangia kwenye alama za maendeleo ya mwanafunzi na hivyo matokeo ya mitihani ya muhula wa kwanza na wa pili ya Kidato cha Tatu nayo yanaweza kutumika kama sehemu ya alama endelevu. Hatua kali zichukuliwe kwa mtu na taasisi yoyote itakayobainika kukiuka maadili katika usimamiaji na uwasilishaji wa matokeo ya mitihani.
Ili kuwaimarisha wanafunzi katika tasnia ya kufikiri na kuandika, kila mwanafunzi afanye project na matokeo yake yatumike kwenye alama endelevu. Projects hizi zianze kuandaliwa wakati mwanafunzi akiwa Kidato cha Tatu na kukamilishwa katika muhula wa kwanza Kidato cha Nne.
Kuhusu muundo wa madaraja, wadau wengi walishauri muundo uliopo sasa wa madaraja uimarishwe ili kuanza kutumia muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Point Average ama GPA). Muundo huu huwa ni rahisi kueleweka na kuuandaa kuliko muundo wa madaraja. Lakini pia, kwa kutumia muundo wa GPA inakuwa rahisi katika kukadiria uwezo wa mwanafunzi kielimu na kufanya maamuzi mbalimbali ikiwemo kuendelea na masomo katika ngazi mbalimbali za elimu.
Mwisho, wadau walikubalianana pendekezo la muundo wa alama lijaribiwe katika mfumo halisi (actual testing) ili kujua faida na athari zake katika mfumo wa elimu kama pendekezo hilo likitekelezwa. Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012 na Kidato cha Sita mwaka 2013 yatumike katika kufanya majaribio na hivyo wataalamu wa mifumo wa NECTA wafanye kazi hiyo na kuleta mapendekezo yao kabla ya uamuzi wa mwisho kufikiwa. Hili lilifanyika (angalia Kiambatansho A Jedwali la 3 na la 4).
Baada ya  majumuisho ya uchambuzi wa maoni ya wadau, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi , Wizara ya Elimu na  Mafunzo ya Amali na Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI walikutana na kushauriana nini kifanyike katika kupanga  viwango  vya alama za mitihani na ufaulu. Katika kikao hicho,  Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara hizo na Kamishna wa Elimu, walipata nafasi ya kupitia maoni ya wadau, kujadili na kupendekeza viwango vipya vya alama za ufaulu vitakavyotumika katika mitihani ya Kidato cha Nne ya mwaka 2013 na Kidato cha Sita ya mwaka 2014. Viwango vilivyopendekezwa  vilizingatia pia maoni yaliyotolewa na wadau hapo juu na hivyo kuridhia kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi sasa itangaze utaratibu wa alama za mitihani ya taifa kwa Kidato cha Nne mwaka 2013 na Kidato cha Sita kuanzia mwaka 2014.

4.    VIWANGO NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA MWAKA 2014 KIDATO CHA SITA
Baada ya kufanya tathmini ya maoni mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa katika maamuzi kuhusu makundi ya alama na muachano wake:
a)    Alama zitakazotumika zitakuwa A, B, C, D, E na F. Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine utafanana, isipokuwa tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna athari za kuwa na muachano tofauti na ule ambao umetumika katika makundi mengine.
b)    Makundi ya alama hayatakuwa na clusters isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta tija katika kupata picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa mantiki hii
(i)     makundi ya alama A, C, D, E na F yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B litakuwa na clusters mbili. Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50 mpaka 59 na litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo wa 50 hadi 59 na kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+ (angalia jedwali hapo chini).
(ii)     Pamoja na kuwa na muachano wa alama 26 kama jedwali linavyoonesha hapo chini, alama A kwa miaka mingi imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na uwigo huo bado wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii, hakuna haja ya kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na ujifunzaji ili kiwango cha ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi zaidi wanaofaulu katika kundi hili.
(iii)     Pia, pamoja na kuwa na muachano wa alama 20 kama jedwali linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko shuleni mwanafunzi aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na ufaulu wa chini kabisa au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa ilikubalika ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha. Alama F ilikuwa ni kwa wale waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na E itaanzia alama 20 hadi 29 na D – 30 -39. Lengo la muundo huu ni kuwa alama mbalimbali, isipokuwa kwa makundi machache, zianzie kwenye 0 yaani 0, 10, 20, 30, 40 na kuendelea badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1, 11, 21, 31, 41 na kuendelea. Hii ni kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana katika ngazi mbalimbali za elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na sekondari zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.
c)    Uwigo wa jumla wa alama kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0 hadi 100 na kila kundi katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi kulingana na malengo ya mtihani husika. Kimsingi, tafsiri zifuatazo zitakatumika
(i)    Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding performance),
(ii)    Alama B+ itakuwa na maana ya ufaulu bora sana (excellent performance),
(iii)    Alama B itakuwa na maana ya ufaulu mzuri sana ( very good perfomance),
(iv)    Alama C itakuwa na maana ya ufaulu mzuri (good performance);
(v)    Alama D itakuwa na maana ya ufaulu wa wastani (low performance),
(vi)    Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na
(vii)    Alama F itakuwa na maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance).
Wataalamu katika maeneo mbalimbali ya elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na Wizara, watatoa maana ya tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana pia na mahitaji yao.
d)    Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alama D na E ni alama za ufaulu unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa anaendelea na masomo ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana na mahitaji ya eneo husika (targeted remediation). Alama F iwe alama ya eneo linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation) ili mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu ama atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.
e)    Makundi ya alama yatajumuisha CA kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea (private candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri izidi uwigo wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.
f)    CA kwa upande wa Kidato cha Nne zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili (alama 15), matokeo ya Kidato  cha Tatu (alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani wa Mock (alama 10) na kazi mradi  au Projects (alama 5). Kwa upande wa Kidato cha Sita, CA iendelee kutokana na muundo unaotumika sasa.
g)    CA zitumike pia kwa watahiniwa wa kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegmea ambao wanarudia Mitihani, CA zao  zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya mitihani ya awali.  Kwa watahiniwa wa kujitegemea waliopitia mfumo wa Qualifying Test (QT), matokeo ya QT yatumike kama CA na mtihani wa mwisho uchangie alama 60.
h)    Kwa vile alama endelevu kwa mwaka 2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari zimeshawasilishwa Baraza la Mitihani  Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2013.
i)    Muundo wa wastani wa alama katika ufaulu (Grade Points Average ama GPA) utaandaliwa na kuanza kutumika pale utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa kuhusu muundo huo ili wapate kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya sekondari.
j)    Muundo huu mpya wa alama utatumika kwa mzunguko wa miaka minne kabla haujahuishwa tena ili kuupa muda wa kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya kuzishughulikia. Aina hii ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya sekondari ya juu kupimwa. Hata hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani unaweza ukafanyika iwapo matokeo ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji pia eneo la mitihani liguswe na kuhuishwa pia.
Kwa mantiki hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini:
Jedwali Na 1
MUUNDO WA ALAMA NA UFAULU
ALAMA    UWIGO WA ALAMA    IDADI YA ALAMA    TAFSIRI
A    75 - 100    26    Ufauli Uliojipambanua
B+    60 - 74    15    Ufaulu bora sana
B    50- 59    10    Ufaulu mzuri sana
C    40 - 49    10    Ufaulu mzuri
D    30 - 39    10    Ufaulu Hafifu
E    20 - 29    10    Ufaulu hafifu sana
F    0 - 19    20    Ufaulu usioridhisha

Kwa aina hii ya muundo wa alama, na kwa kuwa muundo wa GPA utaanza kuandaliwa na wadau kuelimishwa kabla haujaanza kutumika, katika kipindi hiki mpaka wakati huo, muundo wa madaraja utakuwa kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 2 hapa chini.
Jedwali Na 2
MUUNDO WA MADARAJA
MUUNDO WA ZAMANI    MUUNDO MPYA    MAELEZO
POINTI    DARAJA    POINTI    DARAJA   
7-17    1    7-17    I    Kundi la ufaulu uliojipambanua na bora sana
18-21    II    18-24    II    Kundi la ufaulu mzuri sana
22-25    III    25-31    III    Kundi la ufaulu mzuri na wa wastani
26-33     IV    32-47    IV     Kundi ufaulu hafifu
34-35    0    48-49    V    Kundi la ufaulu usioridhisha

Wataalamu wa mifumo ya mitihani watalifanyia kazi zaidi jedwali hili la madaraja ili liweze kutumika kwa ufanisi katika kipindi hiki cha mpito.
Kwa mantiki hii, Daraja Sifuri linafutwa na kuwekwa daraja litakalojulikana kama Daraja la Tano na ambalo litakuwa ndilo la mwisho kabisa katika ufaulu.
5.    HITIMISHO
Mabadiliko haya yamefanyika ili kuendelea kuimarisha mfumo wetu wa elimu na kuweka wazi taratibu mbalimbali kwa ajili ya mitihani na masuala mengine. Yako mambo mengi mengine ambayo hayana budi kuendelea kuimarishwa ikiwemo mfumo wa mitaala, walimu, mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na vitabu na vifaa vingine muhimu katika elimu. Masuala haya yanaendelea kuangaliwa kupitia mikakati mbalimbali ikiwemo mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ama Big Results Now (BRN). Ushirikiano wa wadau wote ili kuleta tija kwenye elimu ni muhimu sana na hivyo wizara itaendelea kuwashirikisha wadau wote kwa kadri itakavyohitajika na wadau pia wanaombwa wasiache kuishirikisha wizara pale watakapokuwa na jambo lolote ambalo linahitaji ushirikiano ili kwa pamoja tuweze kupata mafanikio katika sekta ya elimu.

Imetolewa,

KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni