Ijumaa, 26 Agosti 2016

CCM YAWAUNGA MKONO JESHI LA POLISI

Tokeo la picha la ole sendeka
Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Christopher Ole Sendeka akisisitiza jambo katika mkutano na waandishi  uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam


Timothy Marko.

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeunga mkono kitendo cha Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yanayotarajiwa kufanyika Septemba Mosi mwaka huu kwa kuwa kufanya hivyo kunatokana na hali ya mazingira ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Msemaji wa Chama hicho Christopher Ole Sendeka amesema kuwa Jeshi la Polisi lina mamlaka ya kuzuia mikutano ya kisiasa kutokana hali ya kimazingira.

‘’Sheria ya Jeshi la Polisi kifungu cha 11 na cha 6 cha jeshi hilo kinatoa mamlaka ya kutoa zuio la kutokufanyika kwa mikutano ya kisiasa ama mikutano yoyote kulingana na hali ya kimazingira ya jeshi hilo ‘’Alisema Ole Sendeka.

Ole Sendeka ameongeza kuwa ni vyema watanzania wakaendelea na shughuli za kujiletea maendeleo na kuyapuuza maandamano hayo yanayotarajiwa kufanyika septemba Mosi mwaka huu.

Alisema kuwa chama hicho hakitokubali damu ya watanzania imwagike kwani wamepewa dhamana ya kulinda amani ya nchi ili iweze kustawi..

‘’uhuru unaotolewa na Vyama vya Siasa kufanya siasa una kikomo ,Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuzuia mikutano endapo itaona mikutano hiyo ina lengo la kuhatarisha amani ya nchi , jeshi limepewa mamlaka kuzuia mikutano hiyo ambayo ina viashiria vya uvunjifu wa amani ‘’Aliongeza Ole Sendeka.

Aliongeza kuwa kitendo cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwasiliana na Jumuiya ya Kimataifa juu ya mwenendo wa siasa nchini kimeleta sintofahamu kwa jumuiya ya kimataifa juu ya mwenendo wa siasa hapa nchini.

Olesendeka aliongeza kuwa tayari mashirika ya kimataifa na vyombo vya habari vya kimataifa vimetuma wawakilishi wao kuja kuangalia hali ya kisiasa hapa nchini.

‘’kumekuwa na mashirika ya kimataifa yakiwemo ya CNN na BBC yameshatuma wawakilishi wao kuja kuangalia tukio la Septemba 1 na mwenendo wa sisasa kuhusiana na mandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ‘’Alisisitiza Ole Sendeka.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni