Blogu hii makini iko kwa ajili ya kuhabarisha masuala ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Karibuni sana.
Jumanne, 1 Oktoba 2013
AMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUITAKA SERIKALI KULIFUNGULIWA GAZETI LA MWANAHALISI
Ndugu wanahabari: Ninyi ni mashahidi wa jinsi ambavyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano imekuwa ikijitangaza kwaba inasimamia misingi ya utawala bora nchini. Lakini ninyi nyote mmeshuhudia ambavyo serikali hii imeshindwa kusimamia utawala wa sheria na kuzilinda haki za binadamu.
Majigambo ya serikali kwamba inaheshimu na kusimamia misingi ya demokrasia na utawala bora hayaendani na ukweli halisi. Na hivi sasa, dunia imeanza kushuhudia kuwa wimbo huu unaoimbwa na kuchezwa na serikali hauna ukweli wowote.
Hii ni kwa sababu, leo ni siku ya 175 tangu serikali itangaze kulifungia “kwa muda usiojulikana,” gazeti la kila wiki la MwanaHALISI. Kipindi hiki ni sawa na miezi mitano na siku 24 au miezi sita kasoro siku tano. Huu ni nusu mwaka. Tangu 30 Julai 2012, ilipotangazwa kufungiwa kwa gazeti hilo, wadau wa habari na wananchi wengine kwa ujumla wao; wamekuwa wakipaza sauti kuiomba serikali kulifungulia Mwanahalisi gazeti kipenzi cha wananchi, lakini serikali imekuwa kimya.
Kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi kulitokana na taarifa ambazo zilikuwa na mvuto wa kipekee kuhusiana na kutekwa, kuteswa na kisha kutupwa katika msitu wa Mabwepande, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Dk. Stephen Ulimboka ambaye aliwaongoza madaktari nchini katika kudai maslahi bora, vitendea kazi pamoja na mazingira bora ya kazi.
Masuala kama haya ya kumteka, kumtesa na kumtupa Dk. Ulimboka msituni; na kumfanya nusu mfu; kulifungia gazeti la Mwanahalisi, kuuawa kikatili kwa bomu kwa mwandishi wa kituo cha televisheni cha Chanel Ten, Daudi Mwangosi, kutishiwa kwa watetezi wa haki na mengine mengi, ndiyo yanayotikisa dunia hivi sasa.
Sisi tunaihoji serikali ni lini italifungulia gazeti hili ili wasomaji wake wapate haki yao ya kikatiba ya kupata habari bila kuzuizi? Ni lini serikali itakuwa na huruma na wafanyakazi wa Hali Halisi Publishers Limited, inayochapisha gazeti hili ili kupunguza wimbi la waliokosa ajira nchini?
Kwa namna yoyote ile hakuna taifa linaloweza kusema linapinga ukandamizaji wa uhuru wa kupata habari na kutaka liheshimiwe katika jamii ya kimataifa wakati taifa hilo linaendeleza ukandamizaji wa haki nchini mwake. Tunasema hivyo kwa sababu miongoni mwa viashiria vikuu vya udikteta popote duniani ni pamoja na kuminya uhuru wa vyombo vya habari, na kuwatishia wanaharakati wanapodai haki za raia dhidi ya ukiukwaji wa haki unaofumbiwa na macho na serikali iliyoko madarakani.
Ndugu waandishi wa habari: Kutokana na mazingira hayo, sisi wanamtandao wa watetezi wa haki za binadamu, chini ya mwamvuli wa Tanzania Human Rights Defenders (THRD-Coalition) tunaisihi tena serikali kuurejea uamuzi wake na kulifungulia gazeti la Mwanahalisi. Msimamo huu si wa kikundi fulani bali wa mtandao mzima ambao ni kusanyiko la zaidi ya asasi 60 za kiraia na kwa kushirikiana bega kwa bega na mwanachama mwanzilishi na mwakilishi wa Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika – Tawi la Tanzania (MISA TAN) tunarejea wito wetu wa kuisihi serikali ilifungulie mara moja gazeti la Mwanahalisi na bila masharti.
Leo tunatoa wito huu, tukiwa na sababu za nyongeza, nazo ni kama ifuatavyo:
Kwanza, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema amekiri mbele ya wanahabari kuwa kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dkt. Steven Ulimboka, “Ni siri ya Taifa.” Je, ina maana kuwa kuwa uhai wa Dkt. Ulimboka ni siri ya Taifa? Na je serikali imemkabidhi nani jukukumu lake la msingi la kulinda watetezi wa haki za binadamu kama vyombo husika vinatupiana mpira?
Ndugu wanahabari: Ninyi mnajua kuwa kufungiwa kwa gazeti la MwanaHALISI kulitokana na kuanika kwa ushahidi mwanana usiotia shaka juu ya wanaotajwa kuhusika na utekaji na utesaji wa kiongozi huyo. Aidha, kufungiwa kwa MwanaHALISI kulifuatia hatua ya gazeti kumtaja Bw. Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye aliyehusika na kupanga njama za kumteka na kumtesa Dkt. Ulimboka. Lakini hili pia limethibitishwa na hata Dkt. Ulimboka mwenyewe wakati alipokuwa katika hospitali ya Muhimbili na baadaye aliporejea nchini katika tamko lake lililosomwa na wakili wake.
Hatua ya IGP Mwema kusema suala la kutekwa kwa Dkt. Ulimboka ni “siri ya taifa” na hatua ya Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sulemain Kova kusema “suala la Ulimboka lipo mikononi mwa wakubwa wangu,” yanathibitisha uchunguzi wa MwanaHALISI ulikuwa sahihi.
Ndugu wanahabari: Kutokana na maelezo hayo hapo juu sasa tunaitanabahisha serikali kwa yafuatayo:
a) Rais Kikwete aingilie kati suala hilo kwa sababu, Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda, aliliambia Bunge mjini Dodoma, tarehe 16 Agosti 2012, kwamba “suala la kufungiwa kwa MwanaHALISI liko kwenye mamlaka ya juu ya nchi”
Waziri Mkuu alisema, “Kama kuna mtu yoyote asiyeridhika na uamuzi wa kulifungia gazeti la MwanaHALISI akate rufaa katika mamlaka ya juu.” Waziri Mkuu hakusema, MwanaHALISI waende mahakamani. Alitaja mamlaka ya juu, na kwamba mamlaka ya juu ya Waziri Mkuu hayawezi kuwa waziri wa habari. Mamlaka ya juu ya Waziri Mkuu ni Rais. Uamuzi huo wa rais utalisaidia taifa kurejesha heshima na haiba ambayo sasa imetoweka kutokana na uvunjifu wa wazi wa haki za binadamu.
b) Tunataka hili lifanyike sasa kwa sababu, tumepata taarifa kuwa serikali iko mbioni kupeleka muswaada wa sheria ya huduma za vyombo vya habari bungeni bila kuwa na muswada wa sheria ya kupata habari. Sisi tunajiuliza, unawezaje kupeleka mswaada huo, wakati hapohapo, serikali hiyohiyo imelifungia gazeti. Hivyo basi,tunaitaka serikali kabla ya kupeleka mswaada bungeni, kufuta sheria inayokandamiza uhuru wa habari yaani Newspaper Act 1976 - ambayo imetumika kulifungia gazeti la Mwanahalisi na kwa maana hiyo inaweza kuyafungia hata mengine.
Kwa kuwa serikali ya Rais Kikwete imekuwa ikitajwa kuwa ni sikivu tunamsihi asikilize kilio cha watanzania na kuagiza watendaji wake walifungulie gazeti hili kipenzi cha wote mapema iwezekanavyo.
......................................
Tumaani Mwailenge,
Mkurugenzi Mtendaji- MISA-Tan.
sign.png
Onesmo Olengurumwa- Mratibu wa Kitaifa THRD-Coalition
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni