CHAMA cha National League for Democracy (NLD) kimesema kuwa kina dhamira ya kuwafikisha kwenye Mahakama ya Kimatifa ya Makosa ya Jinai (ICC) huko The Hague, Uholanzi marais wastaafu; Benjamin Mkapa na Amani Karume.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho mjini Zanzibar, marais hao wanadaiwa kutumia nguvu kubwa za kijeshi na kusababisha vifo vya wato 60 kisiwani Pemba mwaka 2001 wakiwa madarakani.
Naibu Katibu Mkuu wa NLD Zanzibar, Khamis Haji Mussa aliliambia RAI kwamba utawala wa viongozi hao ulifanya uhalifu dhidi ya binadamu kwa kutumia helikopta na askari wa ardhini kuwamimiminia risasi wananchi wasio na hatia waliofanya
maandamano Januari 26 na 27, 2001 huko Pemba.
Alisema Mkapa, akiwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Dk. Karume akiwa Rais wa Zanzibar, walisababisha mauaji ya halaiki huku akishangaa kwanini hadi sasa hawajachukuliwa hatua za kisheria.
“Waliokufa ni watu. Taasisi za kutetea haki za binadamu zinapaswa kuingilia kati na kuwafikisha mahakamani viongozi hawa na washirika wao.
“Lakini pia Dk. Karume akiwa madarakani, alitumia vibaya madaraka yake kwa kuhodhi ardhi kubwa ya umma akitegemea kulindwa na Katiba mbovu isemayo Rais hatoshitakiwa akiwa madarakani na hata baada ya kuondoka madarakani,” alisema Mussa.
Alishangaa ni kwanini Rais wa Kenya, Uhuru Kenyata na Makamu wake, William Ruto walifikishwa ICC kwa madai ya kusababisha mauaji ya watu mwaka 2008 wakati Mkapa na Karume wakifumbiwa macho.
Alipokumbushwa kwamba wakati mauaji hayo yakitokea Mkapa alikuwa nje ya nchi na aliyemwachia madaraka alikuwa ni Makamu wa Rais, hayati Dk. Omar Ali Juma, alisema kwa mkato kuwa kila kitu kitajulikana mahakamani.
Alisema miaka mingi baadaye, Karume aliamua kukutana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na kumrubuni kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) isiyo na tija kwa Zanzibar na watu wake.
“Alimrubuni kwa ghiliba Maalim ili tu kukwepa mashitaka. Karume akiwa madarakani alijiwekea chini yake Wizara ya Fedha kwa miaka 10 na kumuahidi Maalim kuwa angemsaidia kupata urais wa Zanzibar.
“Miezi sita kabla ya kukutana kwao Ikulu mwaka 2009, Maalim katika mkutano wa hadhara pale Kibandamaiti alisema Karume na familia yake wanafanya ufisadi wa kupora mali, ardhi na fukwe za bahari huku watoto wake wakipata zabuni kinyume na utaratibu. Leo inashangaza eti anasema Karume ni shujaa na Profesa wa siasa!” alisema na kudai hadi leo anayo kanda ya video ya mkutano huo.
Alidai pia kuwa Karume aliyatumia madaraka yake na kuipinda kama si kuivunja Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na ile ya CCM kwa kuleta SUK kumlinda dhidi ya mauaji yaliyotokea Pemba.
RAI lilipotaka kujua kama ana ushahidi wa madai hayo, alisema: “Nimejiandaa vya kutosha kuihakikishia ICC kuhusu hayo yote pamoja na ndugu na jamaa wa waliopoteza familia zao na sasa wanadai fidia.”
Maandamano ya wafuasi wa CUF kupinga ushindi wa CCM Zanzibar Januari 26 na 27 yalikumbana na rungu la dola na kusababisha mtafaruku mkubwa hadi watu kadhaa kwenda ukimbizini nchini Kenya.
Ingawa NLD inawasakama Mkapa na Karume, wadadisi wa masuala ya siasa walidai kuwa walioitisha maandamano yale, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif nao wanapaswa kuwajibika.
“Lipumba na Seif wala hawakwenda kuyaongoza maandamano. Seif alikwenda ughaibuni eti kuwaomba wahisani waache kuisaidia Zanzibar wakati Lipumba alijificha Buguruni (Makao Makuu ya CUF) wakati wafuasi wao wakipambana na nguvu za dola,” alisema mwanachama mmoja wa CUF akitaka na viongozi hao pia wapelekwe the Hague.
Hata hivyo, mwanasheria mmoja mkongwe aliyewahi kuwa mwanachama mwandamizi wa CUF aliliambia RAI kuwa hakuna uwezekano wowote wa Mkapa na Karume kupelekwa ICC.
“Ni uzushi tu na kutaka kufahamika kwa NLD. Huyo kiongozi angepaswa kwanza kufahamu Mkataba wa Roma (Rome Statute) uliounda ICC unasemaje,” alisema mwanasheria huyo.
Alisema Mkataba wa Roma ulianza kisheria Aprili 11, 2002 pale idadi ya nchi wanachama ilipofika 60, na ICC ikaanza utekelezaji rasmi Julai 1 mwaka huo, na kusema: “Kwa mujibu wa mkataba, ICC ina uwezo wa kuchunguza na kupeleka mahakamani matukio ya kihalifu dhidi ya ubinadamu yaliyofanywa baada ya Julai 1, 2002.
“Maandamano na mauaji ya Pemba yalifanyika mwaka 2001 kwa hiyo ICC haina mamlaka ya kusikiliza wala kupokea malalamiko kama hayo.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni