Jumatatu, 7 Machi 2016

RAIS JONH POMBE MAGUFULI AMTEUA JONH WILIAM KIJAZI KUWA KATIBU MKUU KIONGOZI

 Anitha Jonas –MAELEZO,
Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amemwapisha Katibu Mkuu Kiongozi mpya Balozi John William Kijazi.

Sherehe hizo za kuapishwa zimefanyika leo Ikulu jijini Dar es Salaam kufuatia uteuzi uliyofanyika jana baada ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue kumaliza muda wake.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi mpya, Balozi John William Kijazi amemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumuamini na kumteua pia amesema anaelewa majukumu ya katibu mkuu kiongozi katika serikali ikiwemo kusimamia mazingira ya Watumishi, nidhamu kwa watumishi pamoja na kuwa kiungo kikuu katika kumuunganisha Rais na wizara zake halikadhalika kumshauri Rais katika masuala ya utumishi.

“Natarajia kufanya kazi kwa karibu na watendaji wote wa wizara zote wakiwemo mawaziri,makatibu  wakuu na watendaji wengine ili kujua yale yanatokea kwenye wizara zao na kujua yatakayohitaji maamuzi au ushauri katika maamuzi ya mkutano wa Baraza la Mawaziri na maadhimio yake nitayafuatilia kwa kila waziri kwenye eneo kuhakikisha anatekeleza maadhimio hayo,”alisema Balozi Kijazi.

Aidha Katibu Mkuu Kiongozi mpya aliendelea kusema anaelewa kuwa  serikali ya awamu ya tano imedhamiria kusimamia ukusanyaji wa mapato pamoja na kupambana na rushwa hivyo amejipanga kusimamia yote hayo na kuhakikisha utumishi wa umma unakuwa wa kutukuka na wenye tija kwa kuzingatia nidhamu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi aliyemaliza muda wake, Balozi Ombeni Sefue amesema anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwani haikuwa na lazima yeye kuendelea naye lakini aliweza kumpa muda wa kufanya kazi nae. Pia alisema anamtakia Katibu Mkuu Kiongozi mpya kila la heri katika utendaji na atakuwa tayari kumpa ushirikiano kila atakapohitaji.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi mpya alisema  msamiati wa kutumbua majipu maana yake ni kutafuta nidhamu ndani ya serikali na pale ambapo pana kasoro kurekebisha hivyo nae atamsaidia mheshimiwa Rais hilo ili kuleta mafanikio katika taifa kama serikali ya awamu ya tano ilivyodhamiria na kauli mbiu ya HAPAKAZI TU.

Balozi Ombeni Sefue aliteuliwa na Rais Mstaafu wa serikali ya awamu ya nne, Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na baadae kuteuliwa na kufanya kazi na Mheshimiwa Dkt.John Pombe Magufuli katika serikali yake ya awamu ya tano kwenye kipindi cha mpito

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni